| Chapter 15 |
1 |
Siku moja, watoza ushuru na wahalifu wengi walikwenda kumsikiliza Yesu. |
2 |
Mafarisayo na walimu wa Sheria wakaanza kunung`unika: "Mtazameni mtu huyu! Anawakaribisha wenye dhambi, na tena anakula nao." |
3 |
Yesu akawajibu kwa mfano: |
4 |
"Hivi, mtu akiwa na kondoo mia, akigundua kwamba mmoja wao amepotea, atafanya nini? Atawaacha wale tisini na tisa mbugani, na kwenda kumtafuta yule aliyepotea mpaka ampate. |
5 |
Akimpata, atambeba mabegani kwa furaha. |
6 |
Anapofika nyumbani, atawaita rafiki zake akiwaambia, `Furahini pamoja nami, kwa sababu nimempata yule kondoo wangu aliyepotea.` |
7 |
Kadhalika nawaambieni, ndivyo kutakavyokuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya kutubu kwa mwenye dhambi mmoja, kuliko kwa ajili ya watu tisini na tisa wanaojiona kuwa wema, wasiohitaji kutubu. ic |
8 |
"Au mwaonaje? Tuseme mwanamke fulani ana sarafu kumi za fedha, akipoteza moja, atafanya nini? Atawasha taa, aifagie nyumba na kuitafuta kwa uangalifu mpaka aipate. |
9 |
Akiipata, atawaita rafiki na jirani zake akisema, `Furahini pamoja nami, kwa sababu nimeipata ile sarafu yangu iliyopotea.` |
10 |
Kadhalika nawaambieni, ndivyo watakavyofurahi malaika wa Mungu kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja anayetubu." |
11 |
Yesu akaendelea kusema, "Kulikuwa na mtu mmoja mwenye wana wawili. |
12 |
Yule mdogo, alimwambia baba yake: `Baba, nipe urithi wangu.` Naye akawagawia mali yake. |
13 |
Baada ya siku chache, yule mdogo aliuza urithi wake, akasafiri na fedha aliyopata, akaenda nchi ya mbali ambako aliitumia ovyo. |
14 |
Alipomaliza kutumia kila kitu, kukatokea njaa kali katika nchi ile, naye akaanza kuhangaika. |
15 |
Akaomba kazi kwa mwananchi mtu mmoja wa huko naye akampeleka shambani mwake kulisha nguruwe. |
16 |
Alitamani kula maganda waliyokula wale nguruwe, ila hakuna mtu aliyempa kitu. |
17 |
Alipoanza kupata akili akafikiri: `Mbona kuna wafanyakazi wengi wa baba yangu wanaokula na kusaza, nami ninakufa njaa? |
18 |
Nitarudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. |
19 |
Sistahili hata kuitwa mwanao. Nifanye kama mmoja wa wafanyakazi wako.` |
20 |
Basi, akaanza safari ya kurudi kwa baba yake. Alipokuwa bado yu mbali, baba yake alimwona, na kwa moyo wa huruma alimkimbilia, akamkumbatia na kumbusu. |
21 |
"Mwanawe akamwambia: `Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. Sistahili hata kuitwa mwanao.` |
22 |
Lakini baba yake akawaambia watumishi wake: `Haraka! Leteni nguo nzuri mkamvike! Mvisheni pete na viatu! |
23 |
Mchinjeni ndama mnono; tule kusherehekea! |
24 |
Kwa sababu huyu mwanangu alikuwa amekufa, kumbe yu mzima alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.` Wakaanza kufanya sherehe. |
25 |
"Wakati huo kaka yake alikuwa bado shambani. Alipokuwa akirudi na kukaribia nyumbani akasikia vifijo na ngoma. |
26 |
Akamwita mmoja wa watumishi, akamwuliza: `Kuna nini?` |
27 |
Huyo mtumishi akamwambia: `Ndugu yako amerudi nyumbani, na baba yako amemchinjia ndama mnono kwa kuwa amempata akiwa salama salimini.` |
28 |
Huyo kijana mkubwa akawaka hasira hata akakataa kuingia nyumbani. Baba yake akatoka nje na kumsihi aingie. |
29 |
Lakini yeye akamjibu: `Kumbuka! Miaka yote nimekutumikia, sijavunja amri yako hata mara moja. Umenipa nini? Hujanipa hata mwana mbuzi mmoja nikafanye sherehe pamoja na rafiki zangu! |
30 |
Lakini mtoto wako huyu aliyekula mali yako pamoja na makahaba, mara tu alipokuja umemchinjia yule ndama mnono.` |
31 |
Baba yake akamjibu: `Mwanangu, wewe uko pamoja nami siku zote, na kila nilicho nacho ni chako. |
32 |
Ilitubidi kufanya sherehe na kufurahi, kwa sababu huyu ndugu yako alikuwa amekufa, kumbe yu mzima; alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana."` |