| Chapter 24 |
1 |
Jumapili, alfajiri na mapema, wale wanawake walikwenda kaburini wakichukua yale manukato waliyotayarisha. |
2 |
Walikuta lile jiwe limeviringishwa mbali na kaburi. |
3 |
Walipoingia ndani, hawakuona mwili wa Bwana Yesu. |
4 |
Walipokuwa bado wanashangaa juu ya jambo hilo, mara watu wawili waliovaa mavazi yenye kung`aa sana, wakasimama karibu nao. |
5 |
Hao wanawake wakaingiwa na hofu, wakainama chini. Ndipo wale watu wakawaambia, "Kwa nini mnamtafuta aliye hai kati ya wafu? |
6 |
Hayuko hapa; amefufuka. Kumbukeni aliyowaambieni alipokuwa kule Galilaya: |
7 |
`Ni lazima Mwana wa Mtu atolewe kwa watu waovu, nao watamsulubisha, na siku ya tatu atafufuka."` |
8 |
Hapo wanawake wakayakumbuka maneno yake, |
9 |
wakarudi kutoka kaburini, wakawapa mitume wale kumi na mmoja na wengine habari za mambo hayo yote. |
10 |
Hao waliotoa habari hizo kwa mitume ni: Maria Magdalene, Yoana na Maria mama wa Yakobo, pamoja na wanawake wengine walioandamana nao. |
11 |
Mitume waliyachukua maneno hayo kama yasiyo na msingi, hivyo hawakuamini. |
12 |
Lakini Petro alitoka, akaenda mbio hadi kaburini. Alipoinama kuchungulia ndani, akaiona tu ile sanda. Akarudi nyumbani huku akiwa anashangaa juu ya hayo yaliyotokea. |
13 |
Siku hiyohiyo, wawili kati ya wafuasi wake Yesu wakawa wanakwenda katika kijiji kimoja kiitwacho Emau, umbali wa kilomita kumi na moja kutoka Yerusalemu. |
14 |
Wakawa wanazungumza juu ya hayo yote yaliyotukia. |
15 |
Walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Yesu mwenyewe akatokea, akatembea pamoja nao. |
16 |
Walimwona kwa macho, lakini hawakumtambua. |
17 |
Akawauliza, "Mnazungumza nini huku mnatembea?" Nao wakasimama kimya, nyuso zao wamezikunja kwa huzuni. |
18 |
Mmoja, aitwaye Kleopa, akamjibu, "Je, wewe ni mgeni peke yako Yerusalemu ambaye hujui yaliyotukia huko siku hizi?" |
19 |
Naye akawajibu, "Mambo gani?" Wao wakamjibu, "Mambo yaliyompata Yesu wa Nazareti. Yeye alikuwa nabii mwenye uwezo wa kutenda na kufundisha mbele ya Mungu na mbele ya watu wote. |
20 |
Makuhani na watawala wetu walimtoa ahukumiwe kufa, wakamsulubisha. |
21 |
Lakini sisi tulitumaini kwamba yeye ndiye angeikomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu mambo hayo yalipotendeka. |
22 |
Tena, wanawake wengine wa kwetu wametushtua. Walikwenda kaburini mapema asubuhi, |
23 |
wasiukute mwili wake. Wakarudi wakasema kwamba walitokewa na malaika waliowaambia kwamba alikuwa hai. |
24 |
Wengine wetu walikwenda kaburini wakashuhudia yale waliyosema hao wanawake; ila yeye hawakumwona." |
25 |
Kisha Yesu akawaambia, "Mbona mu wapumbavu kiasi hicho na mioyo yenu ni mizito hivyo kusadiki yote yaliyonenwa na manabii? |
26 |
Je, haikumpasa Kristo kuteswa, na hivyo aingie katika utukufu wake?" |
27 |
Akawafafanulia mambo yote yaliyomhusu yeye katika Maandiko Matakatifu kuanzia Mose hadi manabii wote. |
28 |
Walipokikaribia kile kijiji walikokuwa wanakwenda, Yesu akafanya kana kwamba anaendelea na safari; |
29 |
lakini wao wakamsihi wakisema, "Kaa pamoja nasi, maana kunakuchwa, na usiku unakaribia." Basi, akaingia kijijini, akakaa pamoja nao. |
30 |
Alipoketi kula chakula pamoja nao, akachukua mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. |
31 |
Mara macho yao yakafumbuliwa, wakamtambua; lakini yeye akatoweka kati yao. |
32 |
Basi, wakaambiana, "Je, mioyo yetu haikuwa inawaka ndani yetu wakati alipokuwa anatufafanulia Maandiko Matakatifu kule njiani?" |
33 |
Wakaondoka saa ileile, wakarudi Yerusalemu: wakawakuta wale mitume kumi na mmoja na wale wengine waliokuwa pamoja nao, wamekusanyika |
34 |
wakisema, "Hakika Bwana amefufuka, amemtokea Simoni." |
35 |
Basi, hao wafuasi wawili wakawajulisha yale yaliyowapata njiani, na jinsi walivyomtambua katika kumega mkate. |
36 |
Wanafunzi wote wawili walipokuwa wakiwaambia hayo, Yesu mwenyewe akasimama kati yao, akawaambia "Amani kwenu." |
37 |
Wakashtuka na kushikwa na hofu wakidhani wameona mzimu. |
38 |
Lakini yeye akawaambia, "Kwa nini mnafadhaika? Mbona mnakuwa na mashaka mioyoni mwenu? |
39 |
Angalieni mikono na miguu yangu, ya kwamba ni mimi mwenyewe. Nipapaseni mkanione, maana mzimu hauna mwili na mifupa kama mnionavyo." |
40 |
Baada ya kusema hayo, akawaonyesha mikono na miguu. |
41 |
Wakiwa bado katika hali ya kutosadiki kwa sababu ya furaha yao, na wakiwa wanastaajabu, akawauliza, "Mnacho chakula chochote hapa?" |
42 |
Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa. |
43 |
Akakichukua, akala, wote wakimwona. |
44 |
Halafu akawaambia, "Hii ndiyo maana ya maneno niliyowaambia nilipokuwa pamoja nanyi: kwamba ilikuwa lazima kukamilisha yote yaliyoandikwa juu yangu katika Sheria ya Mose na katika vitabu vya manabii na katika kitabu cha Zaburi." |
45 |
Kisha, akaziangazia akili zao ili wapate kuelewa Maandiko Matakatifu. |
46 |
Akawaambia, "Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka wafu, |
47 |
na kwamba ni lazima, kwa jina lake, mataifa yote kuanzia na Yerusalemu yahubiriwe juu ya kutubu na kusamehewa dhambi. |
48 |
Ninyi ni mashahidi wa mambo hayo. |
49 |
Nami mwenyewe nitawapelekeeni yule ambaye Baba aliahidi kumtuma, lakini ngojeni huku mjini mpaka mtakapopewa ile nguvu itokayo juu." |
50 |
Kisha akawaongoza nje ya mji hadi Bethania, akainua mikono yake juu, akawabariki. |
51 |
Alipokuwa anawabariki, akawaacha; akachukuliwa mbinguni. |
52 |
Wao wakamwabudu, wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha kubwa: |
53 |
wakakaa muda wote Hekaluni wakimsifu Mungu. |