| Chapter 15 |
1 |
"Mimi ni mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. |
2 |
Yeye huliondoa ndani yangu kila tawi lisilozaa matunda, na kila tawi lizaalo hulisafisha lipate kuzaa zaidi. |
3 |
Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya ule ujumbe niliowaambieni. |
4 |
Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Tawi haliwezi peke yake kuzaa matunda lisipokaa katika mzabibu hali kadhalika nanyi hamwezi kuzaa matunda msipokaa ndani yangu. ic |
5 |
"Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi yake. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo atazaa matunda mengi, maana bila mimi hamwezi kufanya chochote. |
6 |
Mtu yeyote asipokaa ndani yangu hutupwa nje kama tawi litupwalo nje hata likakauka. Watu huliokota tawi la namna hiyo na kulitupa motoni liungue. |
7 |
Mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, basi, ombeni chochote mtakacho nanyi mtapewa. |
8 |
Baba yangu hutukuzwa kama mkizaa matunda mengi na kuwa wanafunzi wangu. |
9 |
Mimi nimewapenda ninyi kama vile Baba alivyonipenda mimi. Kaeni katika pendo langu. |
10 |
Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama vile nami nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. |
11 |
Nimewaambieni mambo haya ili furaha yangu ikae ndani yenu, na furaha yenu ikamilike. |
12 |
Hii ndiyo amri yangu: pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda ninyi. |
13 |
Hakuna upendo mkuu zaidi kuliko upendo wa mtu atoaye uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. |
14 |
Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru. |
15 |
Ninyi siwaiti tena watumishi, maana mtumishi hajui anachofanya bwana wake. Lakini mimi nimewaita ninyi rafiki, kwa sababu nimewajulisha yote ambayo nimeyasikia kutoka kwa Baba yangu. |
16 |
Ninyi hamkunichagua mimi; mimi niliwachagueni na kuwatuma mwende mkazae matunda, matunda yadumuyo, naye Baba apate kuwapa ninyi chochote mumwombacho kwa jina langu. |
17 |
Basi, amri yangu kwenu ndiyo hii: pendaneni. |
18 |
"Kama ulimwengu ukiwachukia ninyi, kumbukeni kwamba umenichukia mimi kabla haujawachukia ninyi. |
19 |
Kama mngalikuwa watu wa ulimwengu, ulimwengu ungaliwapenda ninyi kama watu wake. Lakini kwa vile ninyi si wa ulimwengu, ila mimi nimewachagueni kutoka ulimwenguni, kwa sababu hiyo ulimwengu unawachukieni. |
20 |
Kumbukeni niliyowaambieni: mtumishi si mkuu zaidi kuliko bwana wake. Ikiwa wamenitesa mimi, watawatesa na ninyi pia; kama wameshika neno langu, watalishika na lenu pia. |
21 |
Lakini hayo yote watawatendeeni ninyi kwa sababu ya jina langu, kwani hawamjui yeye aliyenituma. |
22 |
Kama nisingalikuja na kusema nao wasingalikuwa na hatia; lakini sasa hawawezi kujitetea kwamba hawana dhambi. |
23 |
Anayenichukia mimi, anamchukia na Baba yangu pia. |
24 |
Kama nisingalifanya kwao mambo ambayo hakuna mtu mwingine amekwisha yafanya wasingalikuwa na hatia; lakini sasa wameona niliyoyafanya wakinichukia mimi, wakamchukia na Baba yangu pia. |
25 |
Na hivi ni lazima yatimie yale yaliyoandikwa katika Sheria yao: `Wamenichukia bure!` |
26 |
"Atakapokuja huyo Msaidizi nitakayemtuma kwenu kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi. |
27 |
Nanyi pia mtanishuhudia kwa kuwa mmekuwa nami tangu mwanzo. |