| Chapter 6 |
1 |
Enyi watoto, watiini wazazi wenu Kikristo maana hili ni jambo jema. |
2 |
"Waheshimu Baba na mama yako," hii ndiyo amri ya kwanza ambayo imeongezewa ahadi, yaani, |
3 |
"Upate fanaka na miaka mingi duniani." |
4 |
Nanyi akina baba, msiwachukize watoto wenu ila waleeni katika nidhamu na mafundisho ya Kikristo. |
5 |
Enyi watumwa, watiini mabwana zenu hapa duniani kwa hofu na tetemeko; fanyeni hivyo kwa unyofu wa moyo kana kwamba mnamtumikia Kristo. |
6 |
Fanyeni hivyo si tu wakati wanapowatazama ili mjipendekeze kwao, bali tumikieni kwa moyo kama atakavyo Mungu kwa sababu ninyi ni watumishi wa Kristo. |
7 |
Muwe radhi kutumikia kwa ajili ya Bwana na si kwa ajili ya watu. |
8 |
Kumbukeni kwamba kila mtu mwenye kutenda mema, awe mtumwa au mtu huru, atapokea tuzo lake kutoka kwa Bwana. |
9 |
Nanyi mnaotumikiwa, watendeeni vivyo hivyo watumwa wenu, na acheni kutumia vitisho. Kumbukeni kwamba ninyi pia kama vile wao, mnaye Bwana yuleyule mbinguni, kwake cheo cha mtu si kitu. |
10 |
Hatimaye, nawatakeni muwe imara katika kuungana na Bwana na kwa msaada wa nguvu yake kuu. |
11 |
Vaeni silaha anazowapeni Mungu mpate kuzipinga mbinu mbaya za Ibilisi. |
12 |
Maana vita vyenu si vita kati yetu na binadamu, bali ni vita dhidi ya jeshi ovu la ulimwengu wa roho; tunapigana na watawala, wakuu na wenye nguvu wanaomiliki ulimwengu huu wa giza. |
13 |
Kwa sababu hiyo, vaeni silaha za Mungu ili siku ile itakapofika muweze kuyapinga mashambulio ya adui; na mkisha pigana mpaka mwisho, muwe bado thabiti. |
14 |
Basi, simameni imara! Ukweli uwe kama ukanda kiunoni mwenu, uadilifu uwe kama vazi la kujikinga kifuani, |
15 |
na hamu ya kutangaza Habari Njema ya amani iwe kama viatu miguuni mwenu. |
16 |
Zaidi ya hayo yote, imani iwe daima kama ngao mikononi mwenu, iwawezeshe kuizima mishale ya moto ya yule Mwovu. |
17 |
Upokeeni wokovu kama kofia yenu ya chuma, na neno la Mungu kama upanga mnaopewa na Roho Mtakatifu. |
18 |
Salini daima, mkiomba msaada wa Mungu. Salini kila wakati kwa nguvu ya Roho. Kesheni bila kuchoka mkisali kwa ajili ya watu wote wa Mungu. |
19 |
Niombeeni nami pia ili niongeapo Mungu anijalie cha kusema, niweze kuwajulisha watu fumbo la Habari Njema kwa uthabiti. |
20 |
Mimi ni balozi kwa ajili ya Habari Njema hiyo ingawa sasa niko kifungoni. Ombeni, basi, ili niweze kuwa hodari katika kuitangaza kama inipasavyo. |
21 |
Tukiko, ndugu yetu mpenzi na mtumishi mwaminifu wa Bwana, atawapeni habari zangu zote mpate kujua ninachofanya. |
22 |
Namtuma kwenu awapeni habari zetu mpate kuwa na moyo. |
23 |
Ninawatakieni ninyi ndugu amani, upendo na imani kutoka kwa Mungu Baba na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo. |
24 |
Nawatakia neema ya Mungu wote wanaompenda Bwana wetu Yesu Kristo kwa mapendo yasiyo na mwisho. |