Kutoka (Biblia)
From Wikipedia
Kitabu cha Kutoka ni kitabu cha pili katika Agano la Kale au Biblia ya Kiebrania. (Kitabu cha kwanza ni Mwanzo.) Kwa asili kimeandikwa katika lugha ya Kiebrania, na katika lugha hiyo kinaitwa Schemot, maana yake “majina”. Wengine wanakiita Kitabu cha Pili cha Mose (au Musa) kwa vile inafikiriwa kuwa Mose ni mwandishi wa kitabu hicho. Kwa lugha ya Kiyunani, kinaitwa Exodos, maana yake “kuondoka kwa watu wengi pamoja”.
Kitabu cha Kutoka kina sura arobaini. Sura 1 hadi 18 zinasimulia Waisraeli walivyokombolewa na Mungu kutoka utumwani kule Misri na safari yao mpaka Mlima Sinai. Sura 19 hadi 24 zinasimulia Mungu alivyofanya agano na Waisraeli pamoja na kuwapa mwongozo wa maisha (Amri Kumi na maagizo mengine). Sura 25 hadi 31 zinaeleza utengenzaji wa hema takatifu (au hema la mkutano) na Sanduku la Agano. Sura 32 hadi 34 zinahadithia Waisraeli walivyoasi na kuabudu sanamu ya ndama wakati Mose alipokuwa amekwenda kuzungumza na Mungu mlimani Sinai. Hatimaye, sura 35 hadi 40 zinaeleza maagizo mengine kuhusu hema takatifu.