NASA
From Wikipedia
NASA ni kifupi cha Kiingereza kwa "National Aeronautics and Space Administration" (Mamlaka ya Marekani ya Usafiri wa Anga). Mamlaka hii ilianzishwa 1958. Wajibu wake ni kusimamia miradi ya serikali ya Marekani ya kuendesha utafiti na uchunguzi wa anga. NASA inatawala utengenezaji wa roketi za kurusha vyombo vya angani na vyombo vya angani vyenyewe.
Miradi ya NASA ilianzishwa kutokana na Mshtuko wa Sputnik yaani baada ya Warusi kushtusha dunia kwa kupeleka vyombo vya angani vya kwanza katika mradi wao wa Sputnik. Ulifuatwa na mradi wa "Vostok" ambao tarehe 12. 04. 1961 ulimfikisha Yuri Gagarin angani akiwa mtu wa kwanza huko kwenda angani.
Mradi wa kwanza wa NASA ulikuwa Mradi wa Mercury uliotakiwa kuonyesha ya kwamba wanaanga wanaweza kukaa angani kwa muda fulani. Alan B. Shepard Jr. alikuwa Mwamerika wa kwanza angani kwa muda wa dakika 15; John Glenn alikuwa Mwamerika wa kwanza wa kuzunguka dunia tarehe 20. 02. 1962 kwa chombo cha angani "Friendship 7".
Mradi huo ulifuatwa na Mradi wa Gemini kuanzia mwaka 1965 ulionyesha ya kwamba watu wanaweza kukaa angani kwa muda wa siku kadhaa hata kutekeleza shughuli fulani. Gemini iliandaa Mradi wa Apollo uliopeleka watu wa kwanza mwezi. Chombo cha angani "Apollo 11" kilifikisha wanaanga Neil Armstrong na Buzz Aldrin kwenye uso wa mwezi tar. 20.07. 1969 na kuwarudisha dunia tena.
Kutoka mwanzo ule kuna miradi mingi iliyofuata.