Historia ya Moroko
From Wikipedia
Historia ya Moroko
Contents |
[edit] Moroko ya kale
Habari za kwanza za kimaandishi ni kuhusi Wafinisia waliounda miji yao kwenye pwani za Mediteranea pia za Moroko ya leo. Walikuta Waberber walioendelea kutawala sehemu za ndani. Kuanzia karne ya pili KK ulijitokeza ufalme wa Kiberber wa Mauretania (usichanganye na nchi ya kisasa Mauretania) uliounganisha sehemu kubwa ya Moroko ya kaskazini. Wamauretania wa kale walishirikiana na Dola la Roma hadi kuwa jimbo la dola hili. Eneo la Moroko ya Kiroma liliitwa "Mauretania Tingitana".
Wakati wa kudhoofika kwa Dola la Roma kuanzia mwaka 400 BK eneo la kaskazini lilivamiwa na Wavandali.
[edit] Uvamizi wa Kiarabu
Kuanzia karne ya saba BK Waarabu walifika wakateka Afrika ya Kaskazini yote. Katika karne zilizofuata Waberber waliokuwa Wayahudi, Wakristo au wafuasi wa dini za kiasili wakawa Waislamu. Mwanzoni Moroko ilikuwa sehemu ya milki ya khalifa ya Waomawiyya waliotawala Dameski. Baada ya kupinduliwa kwa Waomawiyya na Waabasiya wa Baghdad mkimbizi Mwarabu Idris ibn Abdallah (788-791) alikusanya makabila ya Waberber na kuunda milki ya kujitegemea. Hii ilikuwa mwanzo wa Maroko kuwa milki ya Kiislamu ya kujitawala.
[edit] Watawala wa kienyeji
Vipindi vya historia husebabiwa kufuatana na familia zilizofuatana za wafalme Waarabu au Waberber.
Moroko ilitawaliwa na familia za (miaka BK)
- Waidrisi (788-974)
- Wamaghrawa (987-1070)
- Wamurabitun (Almoravi)(1073-1147)
- Wamuwahidun (Almohad) (1147-1269)
- Wamarini (1258-1420)
- Wawattasi (1420-1547)
- Wasaadi (1554-1659)
- Waalawi (1666 hadi leo)
[edit] Murabitun na Muwahidun
Wakati wa Wamurabitun utawala wao ulipanuka kusini hadi Mauretania, Senegal na Mali ya leo. Kaskazini walitawala sehemu kubwa ya Hispania ya Kiislamu.
Wamuwahidun waliendelea kupanuka kuelekea Misri lakini baadaye walidhoofika wakapaswa kuwaachia Wahispania Wakristo sehemu za Andalusia.
Athira ya milki ya Moroko iliendelea kupungua hadi Hispania yote imerudishwa kwa watawala wakristo mwaka 1492; pia utawala kusini ya Sahara haukuendelea. Wareno wa Wahispania waliendelea kuteka miji kwenye pwani za Moroko. Utawala wa Hispania juu ya Ceuta na Melilla hadi leo ni mabaki ya nyakati zile.
Sehemu za nchi zilianza kujitawala bila kukubali tena mamlaka wa juu kwa mfano makabila ya Waberber milimani au miji ya Rabat na Sale iliyounda dola ndogo la Jamhuri ya Bou Regreg katika karne ya 17 BK na kujishughulisha na uharamia zikishambulia hasa jahazi za Wakristo baharini.
[edit] Waalawi (1666 hadi leo)
Katika karne ya 17 familia ya Waalawi walishika mamlaka wakaendelea nayo hadi leo. Waliweza kutunza uhuru wa nchi hadi mwanzo wa karne ya 20 BK. Lakini mwanzo wa karne ya 20 Ufaransa na Hispania walimlazimisha mfalme Moulay Abdelaziz kukubali mkataba uliofanya Moroko kuwa kama koloni chini ya nchi hizo mbili.
Vita Kuu ya Pili ya Dunia ilidhoofisha Ufaransa pamoja na kuingia kwa wanajeshi Waamerika na Waingereza na ahadi zao za kuleta uhuru tokeo lililohamasisha wazalendo wa Maroko kupigania upya uhuru wa nchi. Baada ya vita Wafaransa walijaribu kukandamiza mwendo huo wakamwondoa Sultani Mohammed V nchini 1953. Ghasia ikaongezeka, Sultani Muhammad V akarudi nchi ikapewa uhuri mwaka 1956.
Utawala wa mwanake Hassan II kuanzia mwaka 1961 uliitwa "miaka ya risasi" kwa sababu mfalme alikataa kukubali utaratibu wa kidemokrasia. Uchaguzi zilikuwa za uwongo wapinzani wakatupwa jela au kuuawa. Hassan II alishinda majaribio mbalimbali za kumpindua. Siasa ya kushikamana na Marekani ilimsaidia mfalme kimataifa lakini baada ya mwisho wa "vita baridi" alilazimishwa na Wamarekani kulegea utawala wake.
Mtoto wake Muhamad VI akawa mfalme kijana 1999 akaanza matengenezo ya kisiasa ya wazi zaidi.